Saturday, July 6, 2013

WAKE ZA MTUMEBIBI KHADIJA BINTI KHUWAYLID
(Radhiya Llahuu anha
Jina lake ni Khadija binti Khuwaylid bin Asad bin Abdul Uzza Qusay bin Kilab anayetokana na kabila la Kikureshi aliyezaliwa katika mwaka wa 68 kabla ya Hijra yaani mwaka 556 baada ya Nabii Issa (Alayhis Salaam).
Wazee wake walimlea kwa heshima na adabu ya hali ya juu na alikuwa akijulikana kwa jina la ‘Aliyetakasika’ hata kabla ya kuja kwa Uislamu.
Imepokelewa kuwa siku moja vijana wa kabila la Kikureshi walipokuwa wamekaa karibu na Al Kaaba wakizungumza, aliinuka mmoja wao anayeitwa Al Harith akasema:
“Enyi ndugu zangu nimetia nia ya kuowa”.
Mmojawao akamwambia:
“Uamuzi mzuri huo, kwani tokea alipofariki mama yako na baada ya baba yako kuowa mke mwingine umekuwa unaishi peke yako”.
Mwengine akasema:
“Umefanya vizuri kuamua kuoa, kwani kila mwanamke anatamani kuolewa na mtu kama wewe, maana baba yako ni katika watu wanaoheshimika katika kabila la Kikureshi, na wewe unamiliki mali nyingi sana, sidhani kama yupo mwanamke atakayekukataa”.
Al Harith Akawatizama wenzake kwa muda, kisha akasema:
“Nyinyi mnadhania hivyo kwa sababu ni rafiki zangu, lakini mnakosea”.
“Tunakosea vipi?  Hebu tufahamishe”.
Akawaambia:
“Nilitaka kumuowa Khadija, lakini baba yake alinikatalia kwa sababu eti anasema kuwa kabila langu ni duni kuliko kabila lake”.
Wenzake wakasema:
“Bila shaka hiyo, kwani Khadija ni binti wa Khuwaylid bin Asad naye ni mtu mtukufu miongoni mwa mabwana wa kabila la Kikureshi mwenye kumiliki mali nyingi sana na nyumba kubwa ambayo daima inapokea wageni mbali mbali wanaokuja Makka”.
Mwengine akasema:
“Na Khadija binti yake ni uwa katika mauwa ya Makka, kwani yeye ni mzuri wa umbo na mbora wa mwenendo na tabia, na sifa zake njema pamoja na hekima na uhodari wa kuyapima mambo katika akili yake, vyote hivyo vinajulikana na kila mtu”.
Walipokuwa katika hali ile alipita mbele yao mtu mrefu, mwingi wa haiba aliyevaa nguo zilizoshonwa vizuri na kupambwa, pamoja na kilemba, na nyuma yake kundi la watu lilikuwa likimfuata.
Watu wote walinyamaza kimya huku wakimtazama mtu huyo alipokuwa akipita, kisha mmoja wao akasema kwa sauti ndogo hafifu:
“Huyu ndiye Khuwaylid baba yake Khadija, na walio nyuma yake ni watu wa kabila lake”.
Mwengine akasema:
“Amekuja kutufu Al Kaaba kama kawaida yake ya kila siku”.
Baada ya kutufu Al Kaaba, Khuwaylid akatafuta mahala karibu na Al Kaaba ili aweze kukaa na kujipumzisha, na alipokuwa katika hali ile, kijana mmoja aliiunuka na kwenda kumkabili.
Kijana huyo alikuwa mwenye sura na umbile la kupendeza ambaye kutokana na vazi lake alionyesha kuwa ni mtu tajiri sana, na nyuma yake pia kundi la watu lilikuwa  likimfuata kwa heshima na adabu.
Mtu huyo alikuwa ni Atiq bin Aidh, mmoja katika watu wanaoheshimika miongoni mwa matajiri wakubwa wa kabila la Kikureshi.anayetokana na kabila la Bani Makhzum.
Mmoja katika wale vijana akasema:
“Mtizameni vizuri! Mtu huyu anapigiwa mifano katika ushujaa na ukarimu”.
Baada ya kumkabili Khuwaylid bin Asad, Atiq akamwambia:
“Asubuhi njema ewe Khuwaylid”.
Khuwaylid akamjibu:
“Njema kwako pia ewe Atiq”.
Atiq:
“Nimekuja kwa ajili ya mazungumzo na wewe ewe mwana wa ami yangu, lakini mazungumzo yenyewe hayafai kuzungumzwa hapa penye Al Kaaba mbele ya watu”.
Khuwaylid akamwambia:
“Karibu nyumbani kwangu”.
Siku ya pili yake Atiq akamwendea nyumbani kwake na kumwambia:
“Nimekuja kumposa binti yako ewe bin ami yangu”.
Khuwaylid akamuuliza:
“Umekuja kumposa Khadija au Hala?”
“Bali nimekuja kumposa Khadija ewe bin ami yangu”.
“Vyema, lakini itabidi kwanza nimuulize Khadija mwenyewe ili nijuwe rai yake."
Atiq akasema kwa mshangao:
“Lakini wewe ni baba yake na unanijuwa mimi vizuri na unaijuwa daraja yangu katika kabila la Kikureshi pamoja na mwenendo na tabia zangu”.
Khuwaylid akamjibu:
“Bila shaka ewe bin ami yangu natambuwa yote hayo, natambua vizuri pia kuwa anakustahikia mwanamke yeyote wa Kikureshi, isipokuwa mimi siwezi kuamua lolote juu ya Khadija mpaka kwanza nimuulize mwenyewe na aridhike.”
Atiq akaondoka huku akisema kumwambia Khuwaylid:
“Vyema, fanya hivyo na mimi nitasubiri”.
Baada ya Atiq kuondoka, Khuwaylid akaingia kwa binti yake Khadija na kumjulisha juu ya Atiq, akamwambia:
“Ewe Khadija, kwa hakika Atiq amekuja kukuposa, nini rai yako?”
Khadija akasema kumwambia babake:
“Nini rai yako wewe kwanza ewe baba yangu?”
Baba yake akamwambia:
“Yeye ni bwana katika mabwana wa Kabila la Bani Makhzum na ana mali nyingi sana”.
Bibi Khadija akasema:
“Baba yangu, mimi sikuulizi juu ya sifa hizo, bali nataka kujuwa juu ya sifa zake nyingine kama vile ushujaa na ukarimu na kwamba hawafanyii ubakhili wenye kuhitaji wanapomwendea.”
Baba yake akamwambia:
“Atiq bin Aaidh yuko kama ulivyosema ewe Khadija. Yeye ni shujaa, mkarimu anayependa wageni. Hakika sifa zote unazozitafuta anazo mwanamume huyu”.
Bibi Khadija akasema:
“Basi, ikiwa ni hivyo fanya vile unavyoona wewe kuwa ni sawa ewe baba yangu”.
Bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) akaolewa na Atiq wakapata mtoto waliyempa jina la Hind, na wakaishi kwa wema mpaka alipofariki mumewe jambo lililomfanya Bi Khadija awe na huzuni kubwa.
Haukupita muda mrefu bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akaolewa na Nibash bin Zirarah Al Tamimi aliyekuja kujulikana kwa jina la ‘Abu Halah”,  na wakapata watoto wawili waliowapa majina ya Hind na Halah. Waliishi kwa wema mpaka mumewe wa pili naye pia alipofariki dunia, na haukupita muda mrefu baba yake Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) naye pia akafariki dunia, jambo lililozidisha huzuni moyoni mwake. (zipo riwaya zinazosema kuwa baba yake bi Khadija alifariki dunia baada ya binti yake kuolewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na kwamba yeye ndiye aliyeifunga ndoa yao. Hata hivyo riwaya zenye nguvu zaidi zinasema kuwa alifariki kabla ya bibi Khadija kuolewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na kwamba aliyefunga ndoa ya bibi Khadija na Mtume (Swalla Laahu alayhi wa sallam)alikuwa kaka yake anayeitwa Amru bin Khuwaylid.

Baada ya misiba hiyo iliyofuatiliana, Bibi Khadija aliyerithi mali nyingi sana kutoka kwa baba yake na kutoka kwa waume zake waliofariki, aliamua kujitenga na watu akawa anajishughulisha na ulezi wa wanawe.
Watu wengi walipeleka posa kutaka kumuoa, lakini Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) aliwakataa kwa sababu alihisi kuwa wote hao walikuwa wakimtaka kwa ajili ya tamaa ya mali yake na uzuri wake.
Baada ya kupatwa na misiba miwili hiyo, (kufiwa na mumewe wa pili na kufiwa na baba yake) Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) aliishi akiwa mwingi wa huzuni na mwingi wa kutafakari. alijitenga mbali na watu na aliacha hata kwenda kutufu Al Kaaba kama alivyokuwa akifanya hapo mwanzo.
Inajulikana kuwa Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) hakupata hata siku moja kuyasujudia masanamu yaliyokuwepo hapo, na hii ni siri aliyomjulisha bin ami yake maarufu Waraqah bin Noufel aliyekuwa akifuata dini ya Manasara.
Waraqah bin Noufel huyu alikuwa mcha Mungu sana na alikuwa akisoma sana vitabu vilivyotangulia na kwa ajili hiyo alikuwa akijulikana sana miongoni mwa waarabu wa Makka kwa ucha Mungu wake na wema wake.

Siku moja Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akiwa na uso uliojaa huzuni alikwenda kumtembelea bin ami yake huyo aliyemuuliza:
“Kuna nini binti ami yangu, mbona nakuona una huzuni nyingi?”
Bibi Khadija akamwambia:
“Sijaiona tena furaha tokea alipofariki baba yangu, na mali nyingi niliyoirithi haikuweza kuziba pengo lake”.
Waraqah akamwambia:
“Usihuzunike ewe binti ami yangu, utakuja kuonana naye Akhera”.
Bibi Khadija akashangaa:
“Akhera? Ni kitu gani hicho kinachoitwa akhera ewe bin ami yangu?”
Waraqah:
“Hayo ni maisha baada ya kifo, na katika maisha hayo kila nafsi itapata jaza yake kutokana na yale yaliyotanguliza mikono yake”.
Bibi Khadija akauliza huku akitetemeka:
“Ina maana kuwa baba yangu hivi sasa yuhai?”
Waraqah akamwambia:
“Ndiyo, roho yake iko hai, isipokuwa mwili wake ushachanganyika na udongo wa ardhi”.
Bibi Khadija akaanza kusema huku mwili wake ukiwa unamtetemeka:
“Bin ami yangu, nataka kukupa siri niliyoizuwia moyoni mwangu tokea nilipokuwa mtoto mdogo mwenye umri wa miaka sita”.
Waraqah akasema:
“Sema ewe binti ami yangu wala usiwe na khofu”.
Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akasema:
“Nilipokuwa na umri wa miaka sita hivi, nilikwenda siku moja pamoja na baba yangu penye Al Kaaba nikamuona akisimama mbele ya masanamu yaliyotengenezwa kwa mawe kisha anayakabili na kukiinamisha kichwa chake kwa kuyaheshimu. Nikamuuliza:
“Nini haya masanamu ewe baba yangu?”
Akaniambia:
“Hii ni miungu tunayoiabudu”.
Nikashangazwa nikiwa bado mdogo, vipi watu wanayaabudu mawe yasiyoweza kudhuru wala kunufaisha?”
Waraqah akamtizama Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) huku akitabasamu, kisha akamwambia:
“Uliwahi kumhadithia mtu yeyote katika watu wa nyumbani?”
Bibi Khadija akasema:
“Abadan, abadan. Sijapata kumhadithia mtu yeyote, kwani nilikuwa nikiogopa sana, nikaificha siri hii mpaka nilipokuja kukuhadithia wewe sasa hivi. Nini rai yako ewe bin ami yangu?”
Waraqah akamwambia:
“Huo ndio ukweli wenyewe. Yale ni mawe tu yasiyodhuru wala kunufaisha. Na atatokea katika zama zetu hizi Mtume anayesubiriwa atakayeyavunja masanamu haya na kuondoa ushirikina na uonevu katika ardhi”.
Bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) akauliza:
“Na lini atakuja Mtume huyo?”
Waraqah akasema:
“Mwenyezi Mungu ndiye Anayejuwa zaidi, isipokuwa vitabu vinasema kuwa; atatokea Mtume katika wakati huu wetu na yeye ndiye atakayekuwa mwisho wa mitume”.
Bibi Khadija akauliza:
“Na katika kundi lipi atatokea mtume huyo?”
Waraqah akasema:
“Allahu aalam, lakini Mayahudi wanasema kuwa atakuwa katika wao, na vitabu vinasema kuwa atakuwa miongoni mwa Waarabu”.
Bibi Khadija:
“Na uliyajuaje yote haya ewe bin ami yangu?”
Waraqah:
“Haya yameandikwa katika Tuarati kitabu cha Mayahudi na katika Injili kitabu cha Manasara”.
Bibi Khadija akaondoka hapo huku mawazo yake yote yakiwa juu ya huyo Mtume mpya aliyebashiriwa na bin ami yake atakayeuondoa ushirikina na dhulma na jeuri iliyopindukia mipaka, lakini wakati huo huo mazungumzo hayo yalimsaidia sana katika kupunguza uzito uliokuwepo kifuani pake na huzuni aliyokuwa nayo, na kwa ajili hiyo akaanza tena kufanya shughuli zake za kawaida pamoja na za kibiashara.
Katika shughuli zake za kibiashara bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) alikuwa akiwaajiri wanaume wawili kila mwaka. Mmoja kwa ajili ya kwenda Sham wakati wa Kusi na mwengine kwa ajili ya kwenda Yemen wakati wa Kaskazi. Na hivi ndivyo yalivyokuwa maisha ya kibiashara Bara ya Arabu yote.
Wakati huo huo Muhammad bin Abdillah (Swalla Laahu alayhi wa sallam) (kabla ya kupewa utume) alikuwa akiishi pamoja na ami yake Abu Talib baada ya kufariki kwa babu yake Abdul Muttalib, na alikuwa akimsaidia ami yake katika shughuli za kibiashara na katika kuchunga kondoo na mbuzi mpaka alipofikia umri wa miaka ishirini na mitano, na kutokana na  uaminifu wake na ukweli wake, watu wa Makka walikuwa wakimuheshimu sana.
Hii ukijumuisha pia kuwa Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam) hakupata hata siku moja kuyasujudia masanamu waliyokuwa wakiyaabudu na kuyaogopa wala hakupata kunywa pombe, na hakuwa akijishughulisha na anasa wala starehe ya aina yoyote ile katika starehe walizokuwa wakijishughulisha nazo vijana wa wakati ule.
Alikuwa mwema, msema kweli, muaminifu, mwenye tabia na mwenendo mwema uliompendeza kila mtu, na alikuwa na haiba kubwa sana pale Makka hata akawa maarufu miongoni mwao kwa jina la ‘Al Swaadiqul Amin’, bimaana Mkweli Mwaminifu.au ‘Muhammad Al Amin’, na maana yake ni Muhammad muaminifu.
 
Sifa zote hizo zilikuwa zikimfikia bibi Khadija aliyekuwa mfanya biashara maarufu pale Makka pamoja na sifa nyingine mbali mbali, na pia zilikuwa zikimfikia habari za kusafiri kwake pamoja na ami yake Abu Talib katika shughuli za kibiashara kwenda nchi ya Sham, na kwamba ami yake alikuwa akipata faida kubwa sana tokea alipoanza kushirikiana naye katika shughuli hizo.
Habari hizo zikawa zinamshughulisha sana bibi Khadija na usiku mmoja katika siku za joto alipokuwa amekaa juu ya dari la nyumba yake pamoja na mwanamke mmoja aitwae Nafisa binti Munabih, bibi Khadija alikuwa akitazama chini sana huku akitafakari, jambo lililomfanya Nafisa amuulize:
“Unatafakari juu ya nini ewe Khadija?”
Bi Khadija:
“Natafakari juu ya jambo la ajabu sana”.
Bi Nafisa:
“Unanificha mimi?”
Bi Khadija:
“Mimi siwezi kukuficha kitu ewe Nafisa, jambo lenyewe linahusiana na Muhammad bin Abdillah!”.
Bi Nafisa:
“Ah! Muhammad Muaminifu. Unataka nini kwake?”
Bi Khadija:
“Muhammad Muaminifu husafiri baadhi ya wakati kwa ajili ya shughuli za kibiashara pamoja na ami yake Abu Talib, ningefurahi kama angekubali pia kushughulikia biashara zangu maana yeye ni mtu wa pekee ninayeweza kumuaminisha katika mali yangu. Lakini sijuwi vipi nitaweza kumjulisha?”
Nafisa:
“Mimi, mimi ndiye nitakayemjulisha ewe Khadija, lakini nitazungumza na ami yake Abu Talib maana naona haya kumkabili Muhammad juu ya jambo hili.”
Abu Talib akalikubali ombi hilo na akamnasihi Muhammad akubali pia, na Mtume (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) akamwambia ami yake:
“Ikiwa wewe unaona sawa, basi na mimi nimekubali”.
Bibi Khadija alifurahi sana alipojulishwa kuwa Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) amelikubali ombi lake, akatayarisha msafara wa biashara na kumtaka mtumishi wake Maysara afuatane na Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam) kwa ajili ya kumhudumia na kumshughulikia katika safari ndefu hiyo.
Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) akafanikiwa kuuza bidhaa zote za bibi Khadija katika masoko ya Sham na akarudi akiwa amempatia faida kubwa sana kuliko alivyowahi kupata miaka yote iliyopita.
Rudi naye Makka haraka sana
Tokea waliporudi kutoka safari ya Sham yule kijana Maisara aliyevutiwa sana na tabia na mwenendo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alouona walipokuwa safarini, akawa anamuhadithia bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) juu ya yale aliyokuwa akiyaona safarini walipokuwa wakienda na walipokuwa wakirudi na baadhi ya miujiza iliyokuwa ikitokea.
Bibi Khadija naye aliyekuwa wakati wake wote anawaza juu ya Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alikuwa akipenda kila mara kuhadithiwa juu ya sifa zake hizo, na siku moja alipokuwa amekaa pamoja na mtumishi wake huyo, akamwambia:
“Enhe! Hebu nihadithie vizuri juu ya safari yako na Muhammad”.
Maisarah akasema:
“Sikupata kuona mtu bora wa kusafiri naye kuliko yeye. Alikuwa mtulivu, hana kiburi, mkarimu na mpole sana. Nilikuwa ninapoumwa ananishughulikia na ninapochoka ananisaidia, na alikuwa akigawana na mimi sawa sawa chakula chake na maji yake. Kwa hakika alikuwa akinitendea kama kwamba ni ndugu yake.
Lakini jambo lililonistaajabisha zaidi ewe bi Khadija,” akaendelea kusema: “kulikuwa na kiwingu kilichokuwa kikimfuata wakati wote tokea tulipoondoka mpaka tuliporudi. Kilikuwa kikimfuata na kumkinga na juwa kali wala hakuwa akihisi joto hata kidogo wakati wote wa safari.
Isitoshe, Muhammad hapendi kusema sana, na kila tunaposimama kwa ajili ya kupumzika alikuwa akijitenga peke yake na alikuwa akipenda kutizama mbinguni kwa khushuu na mdomo wake ulikuwa daima ukitikisika huku akisema maneno yasiyosikika”.
Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) aliyekuwa na shauku ya kutaka kujuwa zaidi habari za Muhammad akasema:
“Enhe! Kisha? Endelea, nini kilichotokea baadaye?”
Maisarah akasema:
“Tulipokuwa tukirudi Makka, tulisimama mahali muda mdogo kwa ajili ya kujipumzisha, na mimi nikaondoka kwenda kutafuta chakula cha ngamia, na mahali hapo palikuwa na mti mkubwa sana na Muhammad alikaa chini ya mti huo huku akitizama mbinguni kama kawaida yake kama kwamba anatafuta kitu, na karibu na mahali hapo palikuwa na hekalu la mcha Mungu mmoja aitwae Nastwur aliyenijia mimi na kuniuliza:
“Nani huyu kijana aliyekaa chini ya mti ule?”
Nikamwambia;
“Huyu ni kijana anayetokana na mabwana wa kabila la Kikureshi”.
Akaniambia:
“Umeona lolote lisilo la kawaida kutoka kwake?”
Nikamwambia:
“Nimeona kiwingu kikimfuata kikimkinga kutokana na jua kali tokea tulipoondoka na wala hakikumuacha abadan”.
Akauliza tena:
“Macho yake yakoje?”
Nikamjibu:
“Meusi na makubwa na katika weupe wake umo wekundu khafifu ndani yake”.
Akasema:
“Kijana huyu atakuwa na shani kubwa, rudi naye Makka haraka sana, kwani hakupata kukaa chini ya mti huu isipokuwa Nabii”.
Maneno haya yalimtia kizunguzungu bibi Khadija na tokea alipoondoka hapo akawa usiku na mchana hana analowaza isipokuwa juu ya Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam).
Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akaanza kufikiri huku akikumbuka na kuunganisha maneno ya Maisarah na maneno aliyoambiwa na bin ami yake Waraqah bin Noufel, akawa anajisemesha:
“Kwa nini isinipitikie wakati wote huu? Huyu ndiye kijana anayetokana na mabwana wa kabila la Kikureshi anayejulikana kwa ukweli na uaminifu na upole na ukarimu, na Makureshi wote wanamuheshimu na kumtukuza kutokana na kujitenga kwake mbali na tabia zote mbaya walizokuwa nazo vijana wa kabila la Kikureshi na wengineo.
Na huyu ndiye kijana aliyesafiri na mali yangu na kunipatia faida kubwa sana, na huyu ndiye kijana ambaye kiwingu kilikuwa kikimkinga kutokana na juwa kali tokea alipoianza safari yake mpaka aliporudi. Na huyu ndiye kijana ambaye mcha Mungu Nastwur amesema juu yake kuwa atakuwa na shani kubwa akamtaka Maisarah arudi naye Makka haraka sana”.
Bibi Khadija akawa anawaza na kukumbuka yote hayo mpaka akawa na uhakika ndani ya moyo wake kuwa sifa kama hizi haziwezi kumuandama mtu wa kawaida.
Sifa njema kama hizi ambazo si kila mtu anaweza kuwa nazo hazipatikani isipokuwa kwa watu waliochaguliwa na kutakaswa.
Kutokana na yote haya, bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akazidi kujishughulisha na kuwaza juu ya Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam).
Baada ya kuwaza na kufikiri muda mrefu, bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akafikia uamuzi wa kutaka kuolewa na Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam).
“Kwa nini nisimtake Muhammad aniowe? Inagawaje fikra hii ni mfano wa ndoto, lakini ni jambo linalowezekana. Lakini vipi? Nani atakayekubali kunifikishia ombi langu?”
Alipokuwa katika hali ile, mlango ukagongwa.
“Nani anayegonga mlango?”
“Mimi dada yako Halah.”
Bibi Khadija akamkaribisha dada yake.
“Ahlan wa sahlan, karibu ewe Halah”
Halah:
“Ahsante Khadija vipi hali zenu?”
Khadija:
“Hatujambo, ziara hii ya ghafla naona.”
Khadija:
“Bila shaka ewe dada yangu, kwani nimekuja kukujulia hali yako tu”.
Khadija:
“Kuijua hali yangu tu! Mbona unasema maneno ya kiajabu, au kuna jambo unataka kunificha?”
Halah akamtizama dada yake mtizamo wa kuchunguza, kisha akamwambia:
“Abadan, hakuna la kukuficha isipokuwa mchana wa leo ulinichukuwa usingizi nikakuota unatembea mfano wa mtu aliyepotea katika njia ya kiza na nyuma yako sauti inakwambia: “Nenda mbele, nenda mbele”. Nikaona bora nije kukujulia hali yako, ingawaje sijuwi ndoto hiyo tafsiri yake nini”.
Bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) akatabasamu kidogo kisha akasema:
“Kusema kweli mimi siku hizi ninaishi ndani ya mawazo mengi sana.”
Halah:
“Unawaza juu ya nini na wewe upo katika neema kubwa kama hii?”
Khadija:
“Muhammad, ewe dada yangu. Nafikiri juu ya sifa zake na utukufu wake ambao hajapata kuufikia hata mmoja katika watu wa kabila la Kikureshi.”
Halah:
“Na nini mwisho wa fikra hizo?”
Khadija:
“Nataka aniowe”.
Halah:
“Basi muombe akuowe”.
Bibi Khadija akamjibu kwa uoga:
“Naogopa asije akanikataa, kwani yeye ni kijana anayeheshimika kupita vijana wote”
Halah:
“Na wewe pia dada yangu ni mtu mtukufu unayeheshimika na watu wote”.
Khadija:
“Lakini umri wangu mkubwa unaokaribia miaka arubaini, na nishaolewa mara mbili, wakati yeye bado ni kijana mwenye umri wa miaka ishirini na mitano na bado hajapata kuowa. Vipi Muhammad atakubali kumuowa mwanamke aliye na umri sawa na mama yake aliyekwisha olewa mara mbili na ana watoto?”
Halah akasema:
“Nani aliyekujulisha na Muhammad mara ya mwanzo hata ukaweza kumpa mali yako aifanyie biashara?”
Khadija:
“Rafiki yangu mmoja anayeitwa Nafisa”.
Halah:
“Basi Nafisa huyo huyo ndiye atakayeweza kukufikishia ombi lako hilo”.
Kisha Halah akamuaga dada yake na kuondoka
Ziara ya Hala ilikuwa mfano wa ufunguo wa kheri katika nafsi ya bibi Khadija (Radhiya Llahu anha), kwani siku ya pili yake Nafisa alipokuja kumtembelea bibi Khadija, akamhadithia juu ya mazungumzo yaliyopita baina yake na baina ya dada yake Halah, na Nafisa akakubali kuchukuwa jukumu la kulifikisha ombi hilo kwa Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Alipoondoka, Nafisa alielekea moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Abu Talib alipokuwa akiishi Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na alipomuona akamwambia:
“Ewe Muhammad, wewe una umri wa miaka ishirini na tano na mpaka sasa bado hujaowa.”
Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akashangazwa sana na maneno hayo, akamuuliza:
“Kipi kilichokufanya ujishughulishe na jambo hili ewe Nafisa?”
Nafisa:
“Bibi anayeheshimika anataka umuowe, nini rai yako?”
Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam):
“Bibi gani huyo?”
Nafisa:
“Bibi huyo ni Khadija binti Khuwaylid, na wewe unamuelewa vizuri juu ya heshima yake na utukufu wake na sifa zake zote njema”.
Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema:
“Naam, hakika yeye ni mtu anayeheshimika, lakini mimi sina mali hata niweze kumuowa.”
Nafisa;
“Yeye hana haja ya mahari, kwani unajuwa vizuri kuwa yeye hana shida ya mali na anao utajiri mkubwa”.
Muhammad:
“Mimi utajiri haunishughulishi, kwani mali inakuja na kuondoka, na Khadija pia ni mwanamke mzuri wa umbo na tabia na mwenendo, lakini niache nimshauri ami yangu kwanza juu ya jambo hili”.
Ami yake akamwambia:
“Ewe Muhammad, hii ni bahati iliyokujia kutoka mbinguni. Naapa kuwa Khadija ni mwanamke aliyetakasika kupita wote katika Makka na mwenye akili na uwezo wa kupima mambo kupita wote, na mwenye hekima kupita wote na anayetokana na ukoo bora kupita wote. Wangapi wenye mali na jaha walitaka kumuoa akawakataa, na leo anakutaka wewe wakati huna mali yoyote, hii ni bahati kubwa.
Kubali ewe mwana wa ndugu yangu, kwani asingekutaka isipokuwa amekuwekea heshima kubwa sana”.
Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akakubali, na bibi Khadija akafanya arusi kubwa sana iliyohudhuriwa na watu wengi, na wanyama wengi sana wakachinjwa siku hiyo na kila muhitaji alifaidika.
Bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) alizaa na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) watoto sita. Wanaume wawili na wanawake wanne. Watoto wa kiume aliwapa majina ya Qassim na Abdullah, aliyekuwa akijulikana pia kwa jina la Al Taher. Na watoto wa kike ni Ruqayyah na Zeinab na Ummu Kulthum na Fatima (Radhiya Llahuu anhunna).
 
Katika mwaka wao wa mwanzo tokea kuoana walijaaliwa kupata mtoto wa kiume waliyempa jina la Qassim, wakafurahi sana, na kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akawa anajulikana kwa jina la ‘Abal Qassim’, na maana yake ni 'baba yake Qassim'.
Lakini Qassim hakuishi muda mrefu, kwani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka miwili, na wazee wake walihuzunika sana, lakini walisubiri na kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Kisha akazaliwa Abdullah aliyefariki pia akiwa mtoto mchanga, kisha Zeinab, kisha Ruqayah aliyefanana na mama yake, kisha akazaliwa Ummu Kulthum, kisha akazaliwa Fatima aliyefanana sana na baba yake hasa katika mwendo na sauti.
Siku moja Bibi Khadija (Radhiya Llah anha) aliingia nyumbani akiwa amemshika mkono mtoto mdogo, akamkabili Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na kumwambia:
“Mtoto huyu nakupa zawadi, mchukuwe, atakusaidia na kukuhudumia”.
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamtizama mtoto yule machoni akaona dalili ya hekima ndani yake, akamuuliza:
“Jina lako nani na ilikuwaje ukatekwa?”
Mtoto akajibu:
“Jina langu ni Zeid bin Harithah, natokana na kabila la Kalbin na nilikamatwa na kundi la mabedui walionileta katika soko la Akadha na kuniuza huko”.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akafurahishwa naye, akawa anampenda na kumkirimu sana, na Zeid naye alikuwa akimpenda sana Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na katika nyakati za usiku pale Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) anapojishughulisha na kutafakari na kuomba, mtoto huyo alikuwa karibu yake kwa ajili ya kumtumikia.
Baba yake Zeid alipopata habari za kutekwa kwa mwanawe na baada ya kuulizia ulizia na kujulishwa kuwa mwanawe alikuwa amemilikiwa na Muhammad bin Abdillah, akaifunga safari ya kuelekea Makka na alipowasili alisimama mbele ya Al Kaaba akasema kwa sauti kubwa:
“Enyi watu wa Makka! Nyinyi ni watu wakarimu mnaohudumia mahujaji na mnaowasaidia mateka. Nimekujieni kwa ajili ya mwanangu aliye mikononi mwenu nataka munirudishie mwenyewe”.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliposikia maneno hayo akatangulia mbele na kumkabili Harithah huku akiwa amemshika mkono Zeid, akainama na kumuuliza:
“Unawajua ni nani hawa?”
Zeid akasema:
“Ndiyo. Huyu ni baba yangu na yule ni ami yangu”.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)akamwambia:
“Basi wazee wako hawa wamekuja kukuchukua ili urudi nao”.
Kisha akamuacha mkono na kumtanguliza mbele yao.
Zeid (Radhiya Llah anhu) akamkabili baba yake na kumwambia:
“Baba yangu, mimi sikubali kuachana na mtu huyu abadan, huyu ni mtu adhimu mwenye moyo mkubwa uliobarikiwa, na kama mmoja wenu ataishi naye siku moja tu, basi hatokubali kuachana naye maisha yake yote.”
Kisha akamkabili Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kumwambia:
“Sitomchaguwa mwengine isipokuwa wewe tu. Wewe ndiye baba yangu na wewe ndiye ami yangu”.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alitokwa machozi ya furaha, akamshika mkono Zeid huku akiyafuta machozi yake, kisha akasogea naye mpaka penye uwanja wa Al Kaaba na kusema kwa sauti kubwa:
“Shuhudieni kuwa Zeid ni mwanangu, ananirithi na mimi namrithi”.
Maneno haya yalimfurahisha sana hata Harithah baba yake Zeid kwa kujuwa kuwa mwanawe si kama ameachwa huru tu, bali amekuwa mwana wa Muhammad Mkweli Mwaminifu. Na hii ilikuwa ndiyo kawaida iliyokuwa ikitumika wakati ule.
 
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akimpenda sana Zeid (Radhiya Llah anhu) hata akawa anajulikana kwa jina la Zeid bin Muhammad mpaka pale ilipoteremshwa aya ya nne ya Suratul Ahzab iliyoharamisha mtu kuitwa kwa ubini usiokuwa wa baba yake.
Mwenyezi Mungu anasema:
“Waiteni kwa (ubini wa) baba zao, maana huo ndio uadilifu mbele ya Mwenyezi Mungu. Na kama hamuwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika dini na rafiki zenu”.
Kisha Mwenyezi Mungu akaharamisha pia mtu kurithiwa na mwanawe wa kupanga (adopted child) katika aya ya 75 ya Suratul Anfal aliposema:
“Na ndugu wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe (katika kurithiana). (Ndivyo ilivyo) Katika kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.”
Katika nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alikuwepo mtoto mwingine wa kiume naye ni Hindu mtoto wa bibi Khadija kwa mume wake wa  pili ’Abu Halah’, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akimpenda sana na akamlea malezi bora, akamuonyesha mapenzi na huruma na alikuwa akimtendea kama anavyowatendea wanawe.
Alipotimia miaka minane, Aly (Radhiya Llah anhu) naye akachukuliwa na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kulelewa katika nyumba ya bibi Khadija (Radhiya Llah anha) kwa ajili ya kumpunguzia ami yake Abu Talib mzigo wa ulezi baada ya ami yake kupata shida mbali mbali.
Bibi Khadija (Radhiya Llah anha) alimpokea Aly (Radhiya Llah anhu) kwa furaha na akamlea na kumuenzi kama anavyowalea na kuwaenzi wanawe.
Siku moja Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alimwambia bi Khadija (Radhiya Llah anha) kuwa anahisi moyoni mwake kama kwamba anatakiwa ende penye pango linaloitwa Ghaari Hiraa nje kidogo ya mji wa Makka.
Bi Khadija (Radhiya Llah anha) akamwambia:
“Haya nenda, lakini pango hilo liko nje ya mji na mimi nakuogopea wewe kubaki huko peke yako”.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
“Usiogope Khadija, kwani Mwenyezi Mungu yuko pamoja nami”.
Baada ya bibi Khadija (Radhiya Llah anha) kumtayarishia chakula pamoja na baadhi ya mahitajio yake, Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akaondoka na kuelekea Ghaari Hiraa kwa ajili ya kukaa huko na kutafakari juu ya Mwenyezi Mungu.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akipenda kwenda pangoni hapo na kukaa kimya huku akitazama juu mbinguni. Alikuwa akiziangalia nyota na sayari, juwa na mawingu, mvua na upepo huku akitafakari na kujiuliza:
“Nani aliyevitengeneza vyote hivi? Bila shaka ipo nguvu kubwa yenye uwezo wa kuumba uhai pamoja na kuvitengeneza vyote hivi”.
Akawa anaendelea katika hali hii ya kutafakari wakati mkewe bi Khadija (Radhiya Llah anha) akibaki nyumbani na kuendesha shughuli zake. Lakini bibi Khadija alikuwa kila anapomfikiria mumewe akiwa peke yake pangoni tena nje ya mji alikuwa wakati wa mchana hana raha na wakati wa usiku hapati usingizi.
Alikuwa kila siku akimtuma mtu kwenda pangoni huko ili amletee habari za Muhammad na pia kwa ajili ya kumpelekea maji na chakula na baadhi ya mahitajio yake, na mara nyingine alikuwa akienda yeye mwenyewe.
Siku moja Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alirudi nyumbani kutoka pangoni akiwa na hofu kubwa sana, na bibi Khadija alipomuona katika hali ile akamuuliza:
“Kuna nini Muhammad?”
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
“Ewe Khadija! Nilipokuwa nikitembea huku na kule juu ya jabali, ghafla nikaona nuru iking’ara juu yangu kisha nikasikia sauti ikiniita:
“Ewe Muhammad, ewe Muhammad”.
Bibi Khadija akamuuliza:
“Na umeweza kujuwa sauti hiyo inatokea wapi ewe Abal Qassim?”
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
“Sikuweza kujuwa ewe Khadija, na nilikuwa kila ninapoisikia sauti ninageuka huku na kule kumtafuta mwenye sauti hiyo na wala simuoni mtu, nikaingiwa na hofu na kuamua kurudi nyumbani”.
Bibi Khadija akafanya haraka kumwendea bin ami yake Waraqa bin Noufel na kumhadithia yote aliyohadithiwa na Muhammad, na Waraqah akamwambia:
“Ewe binti wa ami yangu, hizi ni bishara njema kutoka mbinguni, mpe hongera zangu Muhammad na mwambie awe mvumilivu”.
Muhammd (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akawa anaendelea kwenda Ghaari Hiraa, na bibi Khadija (Radhiya Llah anha) akawa anaendelea kumshughulikia kwa kuwatuma watumishi wampelekee vyakula na mahitajio yake ya kila siku na wakati mwingine yeye mwenyewe alikuwa akienda kumtembelea mumewe pangoni mpaka ilipofika siku ile aliporudi nyumbani Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akiwa anatetemeka huku meno yake yakigongana na kumwambia mkewe:
Zammiluni zammiluni’ – na maana yake (nifunikeni, nifunikeni). Bibi Khadija akamlaza mumewe kitandani kisha akamfunika huku akimpangusa  jasho lililokuwa likimtoka kwa wingi kichwani na huku akimwambia maneno ya kumtuliza mpaka usingizi ulipomchukuwa.
Aliamka akiwa bado uoga unaonekana usoni pake na bibi Khadija akamuuliza:
“Una nini ewe Abal Qassim?”
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
“Nilikuwa nimekaa pangoni, ghafla nikaona nuru juu yangu iliyonipitia kama umeme, kisha nikamuona mtu anateremka kutoka mbinguni huku akinikaribia. Nikaingiwa na khofu, lakini mtu huyo akaninyanyua na kunibana kwa nguvu kifuani pake kisha akaniacha, kisha akaniambia:
Iqra-a” – (‘soma’)
Nikamjibu kuwa mimi sijuwi kusoma. Akaninyanyua tena na kunibana kwa nguvu zaidi kifuani pake kisha akaniacha na kuniambia tena:
“Iqra-a”
Nikamwambia:
Maa – ana biqaarii – (Mimi sijuwi kusoma).”
Kisha akaninyanyua tena mara ya tatu na kunibana tena kifuani pake kisha akaniacha akaniambia tena:
اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ {1} خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ {2} اقْرَأْ وَرَبُّكَ
الْأَكْرَمُ {3} الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ {4} عَلَّمَ الْإِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ {5}
(Soma kwa jina la Mola wako Aliyekuumba. Amemuumba mwanaadamu kwa pande la damu. Soma, na Mola wako ni Karimu sana. Ambaye amefundisha kwa msaada wa kalamu. Amemfundisha mwanaadamu mambo aliyokuwa hayajui).
Al Alaq – 1-7
Maneno hayo yalimshituwa sana bibi Khadija, akamtaka Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) avae nguo haraka na afuatane naye mpaka kwa Waraqah bin Noufel ili amhadithie mwenyewe yale aliyoyaona, na Waraqah akamwambia:
“Huyu ndiye Malaika mkubwa ‘Jibril’ ambaye Mwenyezi Mungu aliwateremshia Musa na Issa, yareti kama ningeliishi mpaka pale watu wako watakapokutoa nchini kwako”.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamuuliza:
“Hivyo watakuja kunitoa?”
Waraqah akasema:
“Ndiyo, hapana aliyekuja na haya uliyokuja nayo wewe isipokuwa lazima atafanyiwa uadui, na nikijaaliwa kuishi mpaka siku hiyo, basi nitakusaidia mpaka utakapopata ushindi”.
 
Bibi Khadija akarudi nyumbani haraka akiwa amefuatana na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) huku moyoni mwake akiona fahari kubwa kuwa baraka za utume zimeangukia nyumbani kwake.
Siku moja bibi Khadija aliingia nyumbani kwake na kumuona Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akitetemeka mwili mzima juu ya tandiko lake huku akisema:
“Khadija. Jibril amenijia tena, akaniambia:
يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ {1} قُمْ فَأَنذِرْ {2} وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ {3} وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ {4}
وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ {5} وَلَا تَمْنُن تَسْتَكْثِرُ {6} وَلِرَبِّكَ فَاصْبِرْ {7}
“Ewe uliyejifunika maguo. Simama uonye (viumbe). Na Mola wako umtukuze. Na nguo zako uzisafishe. Na mabaya yapuuze. Wala usiwafanyie ihsani(viumbe) ili upate kujikithirishia (wewe hapa duniani). Na kwa ajili ya Mola wako fanya subira (kwa kila yatakayokufika).”
(Suratul Mudathir aya ya 1 mpaka 7)
Bibi Khadija (Radhiya Llah anha) akainua uso wake kutizama juu mbinguni huku akimshukuru Mola wake, kisha akamtizama Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliyekuwa akionyesha kuwa amechoka sana na kumwambia:
“Tulia upumzike ewe Muhammad”.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
“Zimekwisha zama za kupumzika ewe Khadija. Na umewadia wakati wa jihadi. Jibril keshanijia na ananitaka niianze kazi ya kuufikisha kwa watu ujumbe wa Mwenyezi Mungu utakaouondoa ushirikina pamoja na uchupaji wa mipaka.”
Bibi Khadija (Radhiya Llah anha) akamwambia mumewe:
Labbayka ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, na mimi ni wa mwanzo kukuamini”.
Akasilimu bibi Khadija pamoja na wanawe wote wakiwemo Aly na Zeyd (Radhiya Llah anhum), lakini haukupita muda mrefu Waraqa bin Noufel alifariki dunia kabla ya kupewa utume Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) jambo lililomhuzunisha sana bibi Khadija, kwani Waraqah alikuwa akiwasaidia sana katika kumliwaza Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) wakati wa hofu, na kwa ajili hiyo bibi Khadija akahisi kuwa mzigo huo sasa umemuangukia yeye.
Hata hivyo bibi Khadija alikuwa akimsaidia sana Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pale anapoona dhiki, hasa katika zile siku ambazo wahyi unakatika na Jibril anachelewa kumshukia, hapo Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) humwendea bibi Khadija na kumsikitikia na bibi Khadija kwa upande wake humpoza na kumwambia:
“Hapana ewe Muhammad. Wallahi Mwenyezi Mungu hawezi kukuhizi abadan, kwani wewe ni mkweli muaminifu, uliyetakasika mwenye kuwaendea watu wako na mwenye kuwasaidia wenye kuhitaji na kumuokoa mwenye dhiki”.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akawa anaendelea kwenda pangoni kwa kufanya ibada zake, na mara nyingi Jibril (Alayhis Salaam)  alikuwa akimjia.
Imepokelewa kutoka kwa Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu) kuwa asubuhi moja bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) alipokuwa njiani kuelekea pangoni alikutana na mwanamume mmoja aliyemsalimia na kumuuliza juu ya Muhammad. Bibi Khadija hakumjibu mtu huyo akihofia asije kuwa adui anayeweza kumdhuru Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam). Ikajulikana baadaye kuwa huyo alikuwa Jibril katika sura ya kibinadamu. Kwani Jibril alitangulia kufika pangoni kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na kumwambia:
“Khadija sasa hivi atawasili akiwa amebeba chakula na maji kwa ajili yako. Atakapowasili mpe salamu zitokazo kwa Mola wake na mpe bishara njema juu ya nyumba aliyokwishajengewa Peponi”.
Baada ya kutaabika njiani, bibi Khadija aliwasili pangoni na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alimpokea kwa furaha huku akimwambia:
“Bishara njema kwako ewe Khadija. Amenijia Jibril hivi punde na amenipa salamu zitokazo kwa Mola wako Anayekupa bishara njema juu ya nyumba uliyokwishajengewa huko Peponi”.
Watu wakaanza kuingia katika dini ya Kiislamu kwa wingi, na Abubakar (Radhiya Llahu anhu) alikuwa wa mwanzo katika wanaume akifuatiliwa na Uthman bin Affan, Al Zubeir bin Awaam, Abdul Rahman bin Auf, Saad bin Abi Waqaas na Talha bin Ubaidullah (Radhiya Llahu anhum). Wote hawa walisilimishwa na Abubakar siku ya mwanzo baada ya kusilimu yeye mwenyewe, akaenda nao kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam), na wote hawa ni katika wale kumi waliobashiriwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) kuwa wataingia Peponi.
Siku iliyofuata Abubakar (Radhiya Llahu anhu) aliwasilimisha vigogo wengine wanne na kuja nao mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam), nao ni Uthman bin Madha-un, Abu Ubaidah Aamir bin Al Jarraah, Abu Salama na Al Arqam bin Abi l Arqam.
 
Bibi Khadija naye aliitumia mali yake yote katika kuunusuru Uislam, na kwa ajili hiyo nguvu ikaanza kuongezeka kidogo kidogo jambo lililowaghadhibisha sana Makureshi, wakaamua kuwazunguka na kuwapiga pande Waislamu muda wa miaka mitatu na kuwazuwia wasiweze kununua chochote, hata chakula. Ukawapitikia Waislamu wakati mgumu sana mpaka wakawa wanakula majani ya miti.
Waislamu wakahamia katika nyumba za Abu Talib, na bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) alikuwa wakati mwingine akihatarisha maisha yake kwa kununua chakula na kuwapelekea kwa siri.
Haukupita muda mrefu tokea kumalizika kupigwa pande huko alifariki dunia Abu Talib ami yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam), na miezi miwili baadaye akafariki mama wa Waislamu Bibi Khadija binti Khuwaylid (Radhiya Llahu anha) katika mwaka uliokuja kujulikana kama ‘mwaka wa huzuni’ kwa sababu katika mwaka huo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alifiwa na wapenzi wake wawili hao waliokuwa wakimsaidia sana na kumkinga.
.
Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akiwa na umri wa miaka sitini na mitano alifariki katika mwezi wa Ramadhani mwaka wa kumi tokea Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) kupewa utume. Zipo riwaya zinazosema kuwa alifariki miaka mitatu kabla ya Hijra na riwaya nyingine zinasema miaka minne na nyingine zinasema mitano, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) mwenyewe ndiye aliyeteremka kaburini na kumzika na wakati huo hakukuwa na Swala ya maiti.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) hakupata kumpenda yeyote kati ya wake zake kama alivyompenda bibi Khadija (Radhiya Llahu anha), na hakuoa mke mwingine mpaka alipofariki bibi Khadija.
Ingawaje baadaye alioa wake wengi akiwemo bibi Aisha binti Abubakar (Radhiya Llahu anha) aliyekuwa akipendwa sana kupita wake wenzake wote, lakini hakupata bahati aliyoipata bibi Khadija.
Hebu tumsikilize bibi Aisha mwenyewe (Radhiya Llahu anha) akituhadithia.
Anasema Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha):
“Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alikuwa daima akimtaja Khadija, na siku moja alikuja kututembelea Halah dada yake Khadija nyumbani kwetu Madina, na sauti yake ilikuwa imefanana sana na sauti ya Khadija, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alipoisikia tu sauti yake akasema:
“Allahumma huyu ni Halah dada yake Khadija mfungulie mlango upesi”.
Anasema bibi Aisha:
“Nilimuonea wivu Khadija nikasema kumwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu:
“Nakuona unampenda sana Khadija, huachi kumtaja kila siku kama kwamba hapana mwanamke mwengine duniani isipokuwa yeye. Khadija hakuwa na chochote cha zaidi isipokuwa alikuwa mwanamke mzee, na Mwenyezi Mungu amekwishakupa aliye bora kuliko yeye”.
Anaendela kusema bibi Aisha;
“Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alinikiasirikia sana siku hiyo kwa kauli yangu ile akaniambia:
“Hapana wallahi! Hakunipa aliye bora kuliko yeye, kwani yeye aliniamini wakati watu waliponikadhibisha na akanisaidia kwa mali yake wakati watu waliponinyima, na kupitia kwake akaniruzuku watoto”.
Anasema bibi Aisha (Radhiya Llahu anha):
“Nikajisemea moyoni mwangu; 'sitomsema tena vibaya Khadija.”
 
Na katika hadithi nyingine anasema bibi Aisha (Radhiya Llahu anha):
“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) alikuwa anapochinja mbuzi daima akipeleka nyama kwa marafiki wa Khadija, na siku moja nilimuuliza kwa nini anafanya hivyo, akanijibu:
“Mimi nawapenda wote alokuwa akiwapenda”.
 
Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) alikuwa wa mwanzo kupita wote kumuamini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam), na wa mwanzo kusilimu miongoni mwa wanawake na wanaume, na wa mwanzo kuswali nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) wakiwa peke yao nyumbani.
Alikuwa mara nyingi akimliwaza na kumtuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) anapodhikika au anapoadhibishwa au kukadhibishwa au kutukanwa au anapopata mateso ya aina yoyote kutoka kwa makafiri wa Makka.
1-     Mtu asivunjike moyo hata kama ana tumaini dogo namna gani, kwani bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) aliliona tumaini ndani ya Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) pale alipokuwa akizihesabu sifa zake tukufu moja baada ya nyingine, akiwa na tumaini kuwa mtu huyu ndiye atakayekuwa Mtume anayesubiriwa, juu ya kuwa hizo zilikuwa ni fikra njema tu, lakini hatimaye zikageuka kuwa ukweli halisi.
Alipotamani kuolewa naye, aliliona tumaini lake kuwa mfano wa ndoto, lakini hakuiacha iwe ndoto, bali alizindukana na kuifuatilia ndoto hiyo mpaka ikageuka kuwa kweli.

2-     Mwenendo wa makafiri wa kuwazunguka Waislam na kuwapiga pande na kuwafanyia vikwazo vya kiuchumi na vya kibiashara na kuwaacha wakiwa na njaa wakidhani kuwa mwisho wake watakuja kuwapigia magoti. Darsi hii inatufundisha kuwa mila za kikafiri ni namna moja tokea wakati wa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) mpaka wakati wetu huu.

3-     Mstahamilivu hula mbivu. Waislamu walistahamili kila aina ya tabu na adhabu, mateso na uadui uliokuja kutoka sehemu mbali mbali za ulimwengu tokea siku ya mwanzo, lakini ustahamilivu wao huo haukupotea bure, kwani hatimaye waliweza kupata dola yao na kupambana na adui zao waliokuja kuwapiga vita kutoka kila pembe ya dunia na kupata ushindi wa nyumba mbili. Nyumba ya dunia na nyumba ya Akhera.

 BIBI AISHA
(Rahdiya Llahu anha
Jina lake ni Aisha binti Abubakar Al Siddique (Rahdiya Llahu anha) na jina la mama yake ni Um Ruman bint Amer (Rahdiya Llahu anha).
Aliposwa na Mtume (Swallahu alayhi wa sallam) akiwa na umri wa miaka sita na akamuoa baada ya Hijra, walipohamia Madina akiwa na umri wa miaka tisa, jambo ambalo kwa wakati ule lilikuwa ni la kawaida kabisa katika sehemu hiyo ya ulimwengu.
Bibi Aisha (Rahdiya Llahu anha) alikuwa na kipaji cha elimu, mwingi wa hekima, na kwa kupitia kwake zimepokelewa hadithi za Mtume (Swallahu alayhi wa sallam) zaidi ya elfu moja.
Imepokelewa katika hadithi sahihi kuwa Mtume (Swallahu alayhi wa sallam) alioteshwa mara tatu kuwa anajiwa na Malaika na kuoneshwa uso wa Bibi Aisha (Rahdiya Llahu anha) akiambiwa kuwa huyo ndiye atakayekuwa mkewe. Na Mtume (Swallahu alayhi wa sallam) akawa anasema:
"Ikiwa jambo hili ni kweli, basi Mwenyezi Mungu atalidhihirisha".
Mtume (Swallahu alayhi wa sallam) alikuwa akimpenda sana Bibi Aisha (Rahdiya Llahu anha) na aliwahi kutamka hayo mara nyingi mbele ya baadhi ya Sahaba wake (Rahdiya Llahu anhim), na Masahaba walikuwa wanapotaka kumpelekea Mtume (Swallahu alayhi wa sallam) zawadi, walikuwa wakitegea siku za zamu yake Bibi Aisha, jambo lililowafanya baadhi ya wake wenzake kuona wivu.
Siku moja wake wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) walikutana kwa ajili hiyo na kumtaka Ummu Salama (Rahdiya Llahu anha) amsemeshe Mtume (Swallahu alayhi wa sallam) juu ya jambo hilo ili watu wasiwe wanazihusisha siku za zamu ya Bibi Aisha (Rahdiya Llahu anha) tu peke yake katika kuleta zawadi.
Ummu Salama (Rahdiya Llahu anha) aliufikisha ujumbe huo kwa Mtume (Swallahu alayhi wa sallam), na Mtume (Swallahu alayhi wa sallam) alimnyamazia Ummu Salama (Rahdiya Llahu anha) mara mbili, lakini aliporudia mara ya tatu akamwambia:
"Ewe Ummu Salama, tafadhali usiniudhi juu ya Aisha, mimi wallahi sikupata kuteremshiwa wahyi nikiwa nimelala na yeyote kati yenu hata siku moja, isipokuwa ninateremshiwa ninapokuwa kwa Bibi Aisha".
Bukhari na Muslim na wengineo.
Imepokelewa kutoka kwa Annasai na Attirmidhiy kuwa Mtume (Swallahu alayhi wa sallam) aliulizwa na Amru ibnul Aas (Rahdiya Llahu anhu):
"Yupi unayempenda zaidi kupita wote?"
Mtume (Swallahu alayhi wa sallam) akasema:
"Aisha".
Akamuuliza tena:
"Na katika wanaume je?"
Akasema:
"Baba yake".
Bibi Aisha (Rahdiya Llahu anha) alipata bahati ya kuwa mtu wa mwisho kuchanganya mate yake na mate ya Mtume (Swallahu alayhi wa sallam).
Anasema Bibi Aisha (Rahdiya Llahu anha):
"Mtume (Swallahu alayhi wa sallam) amefariki dunia katika siku yangu (zamu yangu) na akiwa juu ya tandiko langu, na Mwenyezi Mungu amejaalia kuwa jambo lake la mwisho ni kuchanganyika mate yake na yangu. Alipoingia ndugu yangu Abdurahman akiwa amebeba msuwaki mkononi mwake, na Mtume (Swallahu alayhi wa sallam) alikuwa amelala anaumwa sana. Alipofunua macho yake, akawa anautizamatizama msuwaki ule, nikajuwa kuwa anautamani, nikamuuliza:
"Niuchukuwe, unautaka?"
Akatikisa kichwa chake kunijulisha kuwa anautaka.
Nikauchukuwa na kuuingiza mdomoni mwake, akashindwa kuutafuna kwa sababu ulikuwa mgumu, nikamuuliza: 'Nikulainishie?'
Akatikisa kichwa chake akimaanisha; 'Ndiyo'.
Nikauchukuwa kutoka mdomoni mwake nikautafunatafuna kwa ajili ya kumlainishia na alipousogeza uso wake karibu yangu nikaurudisha tena kinywani mwake.
Karibu yake kulikuwa na kibakuli cha maji, akawa anauingiza mkono wake ndani ya kibakuli hicho huku akisema:
"Laa ilaaha illa Llah, hakika katika kutoka roho kuna maumivu".
Kisha akawa anaunyanyua mkono wake juu huku akisema:
"Bali (nataka kwenda) Kwa Mwenyezi Mungu".
Nikajuwa kuwa anashauriwa, na kwamba hatuchaguwi sisi, (bali anachaguwa kwenda kwa Mola wake).
Bukhari na Muslim
Katika vita vya Tukio la ngamia, Bibi Aisha (Rahdiya Llahu anha) alikuwa Makka kwa ajili ya Hija, na mara baada ya kujulishwa juu ya mauaji ya Uthman (Rahdiya Llahu anhu) na juu ya mfarakano mkubwa uliotokea baina ya Wasilamu, akaamua kwenda Basra kwa ajili ya kutaka kupatanisha, na hii inatokana na kuifasiri kwake aya ya 114 ya Suratul Nisaa aliyokuwa akiipenda sana.
Aya hiyo inasema:
"Hakuna kheri katika mengi wanyoshauriana kwa siri. Isipokuwa (mashauri ya) wale wanaoamrisha kutoa sadaka au kufanya mema au kupatanisha baina ya watu. Na atakayefanya hivi kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu basi tutampa ujira mkubwa".
Lakini kwa bahati mbaya mambo hayakuwa kama alvyotamani yawe, na yakatokea yaliyotokea.
Katika hadithi iliyosimuliwa na Imam Ahmed bin Hanbal, anasema:
"Bibi Aisha alipokuwa akiumwa katika maradhi yake ya mwisho kabla hajafariki dunia, alikuwa amekaa na Abdullahi mtoto wa ndugu yake Abdurahman. Akatokea Ibni Abbas (Rahdiya Llahu anhu) na kugonga mlango akiomba ruhusa ya kuingia".
Bibi Aisha (Rahdiya Llahu anha) akasema:
"Mwache huko huko Ibni Abbas".
Abdullah akasema:
"Ewe mama yangu, Ibni Abbas ni miongoni mwa watu wema na anataka kukusalimia na kukuaga".
Akasema:
"Mruhusu aingie".
Ibni Abbas (Rahdiya Llahu anhu) akaingia, na baada ya kukaa vizuri akasema:
"Bishara njema."
Bibi Aisha (Rahdiya Llahu anha) akasema:
"Kwa ajili gani?"
Ibni Abbas (Rahdiya Llahu anha) akasema:
"Baina yako na baina ya kukutana na Muhammad pamoja Sahibu zake ni kiasi cha kutoka roho yako tu ndani ya mwili wako, na wewe ulikuwa mwanamke anayependwa kupita wote na Mtume (Swallahu alayhi wa sallam), na Mtume hakuwa akipenda isipokuwa chema, na siku (ile tulokuwa safarini katika vita) kilipoanguka kidani chako, Mtume (Swallahu alayhi wa sallam) pamoja na watu wote wakawa wanakitafuta, na maji yalipotuishia ikateremshwa aya ya (kutufundisha namna ya) kutayamam, na wewe ndiye sababu ya kuteremshwa aya hiyo. Na Mwenyezi Mungu ameteremsha kutoka juu ya mbingu saba aya za kukutakasa (kutokana na uongo uliozuliwa), na tokea siku ile Jibril alipoziteremsha aya hizo, zikawa zinasomwa katika kila msikiti usiku na mchana".
Bibi Aisha (Rahdiya Llahu anha) akasema:
"Wacha kunipa sifa zote hizo ewe Ibni Abbas, natamani ningekuwa niliyesahaulika".

Kufariki kwake
Bibi Aisha (Rahdiya Llahu anha) alifariki dunia katika Ramadhani ya kumi na saba, mwaka wa hamsini na nane baada ya Hijra, na akausia azikwe katika makaburi ya Baqii - Madina na aliswaliwa na watu wengi wakiongozwa na Sahaba mtukufu Abu Huraira (Rahdiya Llahu anhu), na watu watano waliteremka kaburini mwake, nao ni Abdullahi na Urwa watoto wa Al Zubair bin Al Awaam kutoka kwa dada yake Asmaa bint Abubakar na walishuka pia Al Qassim na Abdullah watoto wa kaka yake Muhammad bin Abubakar na Abdurahman bin Abubakar.
Umri wake Bibi Aisha (Rahdiya Llahu anha) wakati huo ulikuwa miaka sitini na saba.
UMMU SALAMAH
(Radhiya Llahu anha)
Jina Lake ni Hind binti Hudhaifah bin Mughiyra Al Makhzumiy (Radhiya Llahu anha) anayetokana na kabila la Quraysh, na baba yake alikuwa maarufu sana kwa ukarimu wake miongoni mwa waarabu, hata akapachikwa jina la ‘Zawadi ya wasafiri’, na hii ni kwa sababu wasafiri wanaofikia kwake hawakuwa na haja ya kuchukuwa mzigo wowote katika safari zao kwa sababu kwake, walikuwa wakipata mahitajio yao yote.
Ama mumewe wa mwanzo alikuwa Abdullahi bin Abdil Asad (Radhiya Llahu anhu) aliyekuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia katika dini ya Kiislamu. Alisilimu pamoja na mkewe Ummu Salamah (Radhiya Llahu anha) wakati idadi ya Waislamu ilipokuwa chache sana isiyotimia ishirini.
Idadi ya Waislamu ilipoanza kuongezeka na Makureshi walipoanza kuwatesa na kuwafanyia kila aina ya vitimbi ili wawarudishe katika dini ya kuabudu masanamu, na baada ya Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) kuwataka baadhi yao wahamie Uhabeshi katika Hijra ya mwanzo, Ummu Salama pamoja na mumewe (Radhiya Llahu anhum) walikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuutikia wito huo.
Ummu Salamah na mumewe (Radhiya Llahu anhum) waliihama nchi yao na kwenda kuishi ugenini wakiacha nyuma yao nyumba yao nzuri na kila walichokuwa wakimiliki kwa ajili ya kutegemea malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu Subhanahau wa Taala.
Juu ya ukarimu wa An Najashi Mfalme wa Uhabeshi, na juu ya wema alokuwa akiwatendea wageni wake hao walioihama nchi yao na kukimbilia kwake, lakini shauku ya kurudi Makka mahali ambapo wahyi ulikuwa ukiteremka ilikuwa ikiongezeka kila wakati unaposogea mbele, na shauku yao ya kurudi na kuishi na kuwa karibu na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) aliyekuwepo huko ilikuwa kubwa zaidi.
Ummu Salamah pamoja na mumewe (Radhiya Llahu anhum) walikuwa daima wakifuatilia habari za Makka, na uvumi ukaanza kuwafikia kuwa idadi ya Waislamu imeongezeka huko Makka na kwamba kusilimu kwa Hamza bin Abdul Muttalib na Umar bin Khattab (Radhiya Llahu anhum) kumewapa nguvu Waislamu na kwamba sasa Makureshi wameacha kuwaudhi na kuwatesa.
Uvumi huu uliingiza shauku kubwa sana ya kutaka kurudi Makka ndani ya nyoyo za Waislamu waliokuwepo Uhabeshi, na baadhi yao wakiwemo Ummu Salamah na mumewe Abdullahi wakawa miongoni mwa watu wa mwanzo kurudi.
Lakini mara baada ya kuwasili Makka, walivunjika moyo kuona kuwa yote waliyokuwa wakiyasikia yalikuwa ni uvumi mtupu, na kwamba  kusilimu kwa Hamza na Umar bin Khattab (Radhiya Llahu anhum) kuliongeza ukhabithi wa makafiri wa Makka walioanza kuwaonyesha Waislamu kila fani ya kutesa, na Waislamu wakakabiliwa na masaibu makubwa wasiyopata kuyaona katika maisha yao, jambo lililomfanya Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) awatake Waislamu kuhamia Madina.
Ummu Salamah na mumewe wakawa miongoni mwa watu wa mwanzo kutikia wito huo wa Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) isipokuwa mara hii mambo hayakuwa mepesi kwao.
Hebu tumsikilize Ummu Salamah (Radhiya Llahu anha) akituhadithia yaliyomkuta katika hijra yake hii.
Anasema Ummu Salamah (Radhiya Llahu anha):
“Mume wangu Abu Salamah alipotia azma ya kuhajir kwenda Madina akanitayarishia ngamia, kisha akatusaidia mimi na mwanangu Salamah kumpanda ngamia huyo na kuianza safari yetu hiyo ndefu huku tukienda taratibu, sisi tukiwa juu ya ngamia na yeye akiwa ameshika hatamu zake huku akituongoza na hakuwa akitazama huku wala kule.
Lakini kabla ya kuuacha mji wa Makka, jambo la kusikitisha sana likatokea, pale watu wa kabila langu la Bani Makhzum walipotuona na kutujia na kuuzuwia msafara wetu tusiondoke. Wakamwambia mume wangu Abu Salamah:
“Ikiwa wewe unataka kuondoka, basi unaweza kufanya hivyo, lakini binti yetu huyu utamwacha hapa hapa kwetu.”
Kisha wakanichukuwa kwa nguvu mimi pamoja na mwanangu Salamah, na walipokuwa katika hali ile, watu wa kabila la mume wangu Banu Abdul Asad wakatuona na kutujia na kusema kwa ghadhabu:
“Wallahi hatutokuacheni mumchukue mtoto huyu, kwani mtoto huyu ni wetu na sisi ndio tunayemstahikia zaidi.”
Kisha wakaanza kumgombania mwanangu huyo mbele yangu. Watu wa kabila langu wakawa wanamvuta mkono wake mmoja, na watu wa kabila la mume wangu nao wanamvuta mkono mwingine, kila mmoja akimvuta upande wake kwa nguvu mpaka mkono wake ulipochomoka, ndipo watu wa kabila la mume wangu wakafanikiwa kumchukua.
Kuanzia hapo nikaanza kuishi maisha ya upweke yaliyojaa majonzi, mbali na mume wangu aliyehajir peke yake kwenda Madina, na mbali na mwanangu aliyechukuliwa na watu wa mume wangu akiwa na mkono ulionyofoka.
Ama mimi, nikachukuliwa na watu wa kabila langu Bani Makhzum walionirudisha kwetu baada ya kunitenga na wapenzi wangu wawili hao.
Nikawa kila siku kuanzia wakati wa asubuhi mpaka unapoingia wakati wa magharibi hutoka na kukaa mahali pale yaliponitokea masaibu hayo ya kutenganishwa na mume wangu na kuchukuliwa kwa mwanangu, nikiwa sina kazi nyingine isipokuwa kulia tu mpaka usiku unapoingia.
Nikawa katika hali hiyo karibu mwaka mzima, nikikaa na kujikumbusha ule wakati matukio yale yalipokuwa yakitokea kisha ninalia mpaka unapoingia wakati wa usiku na kurudi nyumbani, mpaka siku ile alipopita mmoja katika jamaa zangu aliyenionea huruma baada ya kuniona katika hali ile, akawaambia watu wa kabila langu:
“Kwa nini hamumuachi masikini huyu ende kuungana na mumewe? Kwa nini mnaendelea kumtenganisha na mumewe?”
Akawa anaendela kuwasemesha mpaka huruma ikaingia nyoyoni mwao, wakaniambia:
“Ukitaka unaweza kwenda kwa mumeo.”.
Lakini vipi nitakwenda kwa mume wangu wakati mwanangu kipande cha ini langu yuko Makka kwa jamaa zake mume wangu watu wa kabila la Bani Abdil Asad?
Nitaishi namna gani mimi nikiwa huko Madina wakati mwanangu yupo Makka nami sijuwi lolote juu yake?
Watu wa kabila langu wakaiona ile huzuni iliyojaa usoni mwangu na kuhisi yale yaliyokuwa yakipita moyoni mwangu, wakaamua kuwasemesha watu wa kabila la Bani Abdul Asad wanirudishie mwanangu, ambao kwa bahati nzuri walikubali.
Sikuweza kustahamili kwa furaha iliyonijaa moyoni mwangu baada ya kurudishiwa mwanangu Salamah na kujuwa kuwa sasa ninaweza kusafiri hadi Madina kwa mume wangu bila kipingamizi chochote, na kwa ajili hiyo nikaamua hapo hapo kuifunga safari bila kungoja wala kutafuta mtu wa kufuatana naye nikiogopa watu wangu au watu wa kabila la mume wangu wasije wakabadilisha fikra zao na kuamua kunizuwia tena mimi au kumzuwia mwanangu nisisafiri naye.
Kwa ajili hiyo nikamtayarisha ngamia wangu na kumbebesha vifaa vyangu vya lazima kwa ajili ya safari ndefu hiyo na kuianza safari ya kwenda kwa mume wangu nikiwa peke yangu bila ya mtu wa kufuatana naye.
Nilipowasili mji wa Tan-iym, mji uliopo nje kidogo na Makka kwa kiasi cha maili tatu, nikakutana na Uthmaan bin Twalha aliyekuwa bado hakusilimu wakati huo, akaniuliza:
“Unaelekea wapi ewe binti wa ‘Zawadi ya wasafiri’?”
Nikamwambia:
“Nakwenda Madina kwa mume wangu.”
Akaniambia:
“Unaye wa kufuatana naye?”
Nikamjibu:
“Hapana Wallahi sina isipokuwa Allah na mwanangu huyu.”
Akaniambia;:
“Wallahi sitokuacha usafiri peke yako abadan, mpaka nikufikishe Madina.”
Akashika hatamu za ngamia wangu na kuianza safari ya kuelekea Madina.
Wallahi sikupata kusafiri na mtu miongoni mwa waarabu aliye mkarimu na mwenye heshima kuliko yeye. Alikuwa pale ninapotaka kuteremka juu ya ngamia, anamkalisha kisha anasogea mbele kidogo ili niweze kuteremka juu yake bila yeye kuniona, na baada ya kuteremka alikuwa akija na kumfunga ngamia na mti, kisha anajisogeza penye mti mwingine ulio mbali na mimi na kulala chini yake akiwa mbali na mimi.
Wakati wa kuanza safari unapowadia, alikuwa akija kumfungua ngamia, kisha ananitayarishia kwa ajili ya kumpanda, kisha anatangulia mbele kidogo ili asinione huku nikimpanda, na baada ya kumpanda ngamia na kukaa sawa juu yake, huja na kumshika hatamu zake na kumuongoza.
Akawa anaendela kufanya hivyo kila siku mpaka tulipowasili  mji wa Qubaa (uliopo mbali kidogo na Madina kwa kiasi cha maili mbili), akaniambia:
“Mumeo yupo katika kijiji hiki cha Amru bin Auf, mwendee kwa baraka za Mwenyezi Mungu.”
Kisha akaniacha na kuianza safari ya kurudi Makka.”

Furaha ilioje waliyokuwa nayo siku hiyo pamoja na vigelegele huku machozi ya furaha yakiwatoka pale Ummu Salamah alipojumuika tena na mumewe pamoja na mtoto wao baada ya kufarikiana muda mrefu, na Abu Salamah (Radhiya Llahu anhu) naye alifurahi kupita kiasi.
Tokea siku ile siku zikapita kwa haraka sana. Vita vya Badar vikapiganwa na Abu Salamah (Radhiya Llahu anhu) alishiriki katika vita hivyo na kurudi Madina pamoja na jeshi la Waislamu wakiwa wamepata ushindi mkubwa mbele ya makafiri.
Kisha vikaja vita vya Uhud, vita ambavyo ndani yake Abu Salamah alipigana kwa ujasiri mkubwa, lakini akajeruhiwa vibaya sana na kupata majeraha makubwa yaliyomsababisha kuumwa kwa muda mrefu.
Asubuhi moja Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) alikwenda kumtembelea Abu Salamah (Radhiya Llahu anhu) aliyekuwa amelala juu ya tandiko lake na hali yake ilikuwa mbaya sana, na alipokuwa mlangoni akitoka nje baada ya kumaliza ziara yake, Abu Salamah akafariki dunia, na Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) akaitwa na kurudi ndani, na kuyafumba macho ya sahibu yake kwa mikono yake miwili, kisha akaunyanyua uso wake mbinguni na kuomba dua ifuatayo:
“Mola wangu mghufirie Abu Salamah madhambi yake, na mnyanyue daraja yake na umjaalie awe pamoja na walio karibu Nawe, umjaalie apate mtu mwema wa kuwalea watoto wake, na utuhgufirie sisi na yeye pia ewe Mola wa ulimwengu, umjaalie nafasi kubwa katika kaburi lake na umuingizie nuru ndani yake.”
Ama Ummu Salamah (Radhiya Llahu anha), baada ya kufariki mumewe yeye alikuwa akiomba dua maarufu inayosema:
“Mola wangu kwako nategemea malipo ya msiba wangu huu.”
Lakini hakuwa akipenda kuikamilisha dua hii aliyofundishwa na mumewe siku ile alipoingia nyumbani na kumwambia:
“Ewe Ummu Salamah, nilimsikia Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) akisema:
“Mtu anapopatwa na msiba kisha akasema: ‘Inna lillahi wa inna ilayhi raajiun, Allahumma indaka ahtasibu musiybati haadhihiy. Allahumma akhlufniy khayran minha.  Na maana yake ni;
“Mola wangu kwako nategemea malipo ya msiba wangu huu, na (nakuomba) Unilipe kilicho bora kuliko (msiba) huu.”
Mtu haombi dua hii isipokuwa Mwenyezi Mungu atampa.”

Hakuwa akipenda kuikamilisha kwa sababu alikuwa akijiuliza;
“Kipi kinachoweza kuwa bora kuliko mume wangu Abu Salamah?”
Lakini alipokumbuka maneno ya mumewe akawa anaiomba dua hiyo kwa ukamilifu.
Watu wote wa Madina walimhurumia sana Ummu Salamah, hasa kwa vile pale Madina hapakuwa na mtu wake yeyote isipokuwa wanawe waliokuwa wengi na wadogo wakati ule, na pia alikuwa akilea mayatima watoto wa ndugu yake aliyefariki.
Kwa ajili hiyo watu wengi wakataka kumuoa, lakini Ummu Salamah aliwakataa wote wakiwemo Abubakar Al Siddique na Umar bin Khattab (Radhiya Llahu anhum), mpaka pale alipokuja kuposwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa Sallam), na Ummu Salamah (Radhiya Llahu anha) akamjibu kwa kumwambia;
“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi nina ila tatu. Kwanza mimi ni mtu mwenye wivu sana, naogopa nisije nikakughadhibisha kisha Mwenyezi Mungu kwa ajili hiyo akaja kuniadhibisha. Pili mimi ni mwanamke niliyekwisha zeeka, na tatu mimi nina watoto wengi.”
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) akamwambia:
“Amma kuhusu wivu wako, namuomba Mwenyezi Mungu akuondolee. Ama kuhusu uzee, hata mimi pia nishazeeka kama wewe. Ama kuhusu kuwa na watoto, basi wanao ni wanangu.”
Ummu Salamah (Radhiya Llahu anha) akakubali kuolewa na Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) na kwa ajili hiyo dua yake ikawa imekubaliwa kwa kulipwa na Mwenyezi Mungu kilicho bora kuliko msiba wa kufiwa na mumewe.
Ummu Salamah (Radhiya Llahu anha) alikuwa mwanamke mzuri wa umbo, mtulivu wa tabia, mwenye akili yenye uwezo wa kupima mambo, na mwingi wa hekima ambaye Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) alikuwa mara nyingi akichukuwa ushauri wake katika baadhi ya mambo.
Katika mwaka wa sita baada ya Hijra, Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) aliondoka Madina kuelekea Makka akiwa amefuatana na baadhi ya Masahaba (Radhiya Llahu anhum) kwa nia ya kufanya Umra, lakini Makureshi walimkatalia  kuingia Makka, na kwa ajili hiyo vita vikali vikataka kuzuka baina yao.
Baada ya mashauriano na majadiliano yaliyochukuwa muda mrefu, Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) akakubali kufanya sulhu kwa kuandikiana mkataba na Makafiri hao, mkataba uliokuja kujulikana kwa jina la ‘Sulhu l Hudaibia.’.
Jambo hilo halikuwafurahisha Waislamu waliokuwa na hamu kubwa sana ya kupambana na Makafiri hao, na pia kwa sababu mkataba huo ulikuwa na baadhi ya shuruti ambazo kwa dhahiri yake hazikuonekana kuwa ni nzuri, ingawaje undani wake kulikuwa na manufaa kwa Waislamu katika siku za mbele.
 Baada ya kumaliza kuandikiana mkataba huo na kupigwa mihuri, Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) akawataka Waislamu wainuke, wachinje wanyama wao na wanyoe nywele zao, lakini hapana hata mmoja kati yao aliyeinuka.
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) akarudia kuwaambia mara tatu:
“Inukeni muchinje wanyama wenu na munyowe nywele zenu,” lakini hapana aliyeinuka kutii amri hiyo wakitarajia kuwa amri ya kupigana jihadi huenda ikateremshwa.
Jambo hilo halikumfurahisha Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) aliyekwenda moja kwa moja mpaka penye hema la mkewe akaingia ndani na kumhadithia Ummu Salamah (Radhiya Llahu anha) juu ya jambo hilo.
Ummu Salamah (Radhiya Llahu anha) akamwambia:
“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, watokee na usimsemeshe yeyote kati yao mpaka utakapomaliza kuchinja na kumwita kinyozi wako akunyoe.”
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) akafanya kama alivyoshauriwa na Mkewe, akatoka na hakumsemesha mtu yeyote mpaka alipomaliza kuchinja na kunyoa, ndipo Masahaba (Radhiya Llahu anhum) walipoinuka na wao pia wakachinja na kuanza kunyoana nywele zao.
Ummu Salamah (Radhiya Llahu anha) alifariki dunia katika mwaka wa hamsini na tisa baada ya Hijra na katika maziko yake aliswaliwa na Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu).
Anasema Ibni Abi Khaythamah kuwa Ummu Salamah (Radhiya Llahu anha) alifariki dunia wakati wa utawala wa Yazid bin Muawiya.No comments:

Post a Comment